What's Trending?

Labels

Ads

Sunday, June 7, 2015

UKAWA WAWAPONDA WAGOMBEA WA CCM WALIOTANGAZA NIA KUGOMBEA NAFASI YA URAIS.



Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa. Picha ya Maktaba.

 
Dar es Salaam. Baada ya wiki nzima ya makada wa CCM kutangaza nia na hatimaye kuchukua fomu za kugombea urais, wapinzani ndio wanaonekana kunufaika zaidi kutokana na wengi kutumia hotuba zao kuelezea

udhaifu wa kila mmoja.

CCM imepanga mwezi mzima, kuanzia Juni 3 hadi Julai 2 kuwa ni muda wa makada wake kuchukua na kurudisha fomu kabla ya vikao vya juu vya chama hicho kukutana kuanzia Julai 12 kuchuja wagombea na baadaye kumpata mmoja atakayesimama kwenye Uchaguzi Mkuu kupambana na wa vyama vingine.

Tayari makada 15 wameshachukua fomu na wengine wanaendelea kuchukua, huku waliochukua wakiwa wameshaanza kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini 30 kila mkoa ili kupata idadi ya wadhamini 450. Wanatakiwa kupata wadhamini kwenye mikoa 15, kumi ya Bara na mitano ya Zanzibar.

Karibu wagombea wote walizungumzia nia yao ya kupambana na rushwa, lakini walilitaja tatizo neno hilo kwa nia ya kuwashambulia baadhi yao huku maneno ya kuponda umaskini, kujisifu kwa utajiri, kukaa madarakani muda mrefu, ufisadi na masuala mengine yakitumika kupondana.

Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyetumia muda mwingi wa hotuba yake kijijini Butiama kuponda makada wote, akiwataja kwa majina kuanzia Edward Lowassa aliyeanza kutangaza nia baada ya kuruhusiwa na chama, Mwigulu Nchemba, hadi Steven Wasira, mwanasiasa mkongwe ambaye alianza kuwa waziri tangu miaka ya sabini.

Makongoro aliwaponda makada watatu waliojitokeza kwenye maeneo matatu ambayo ni matumizi ya fedha yaliyopindukia wakati hawana vyanzo vinavyoeleweka, ahadi zao kabla ya kutoka Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa serikalini kwa muda mrefu bila ya kufanya chochote.

Makongoro alisema viongozi wengi wanamyumbisha mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete na kusema kama wanachama wa CCM wanataka chama hicho kisipotee, wampe nafasi ya kukirudisha kwenye njia.

Mgombea wa CCM anatarajiwa kukumbana na upinzani mkubwa zaidi ya mwaka 2010 baada ya vyama vinne-CUF, Chadema, NLD na NCCR Mageuzi- kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja, huku vyama vingine nikionekana kujikita zaidi kwenye ubunge.

“Kwanza, kwa chama tawala kuwa na watu wengi wanaojitokeza kutaka urais, inaonyesha kuwa CCM haina mgombea,” alisema katibu mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alipoulizwa maoni yake kuhusu hali hiyo ya kupondana.

“Hivyo wanavyopondana ndiyo inathibitisha kuwa hawana mgombea kabisa.

Mgombea wa CCM ndiye atakayenadi sera za chama, sasa kama kila mtu anasema lake na halafu wanapondana, ndiyo mambo hay ohayo ya ahadi za ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’ ambayo hayapo hadi leo.” Mawazo yake yanalingana nay a mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye aliweka bayana kuwa kurushiana kwao madongo ni faida kubwa kwa wapinzani.

“Sisi kama opposition tunasubiri mgombea mmoja ambaye atapambana na wagombea wa vyama vya upinzani,” alisema Zitto ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo.

“Lakini kinachoendelea sasa CCM ni advantage kwa wapinzani kwa sababu wanachofanya ni kuonyesha kila mmoja ana udhaifu. Kwenye uchaguzi, wnasiasa wanaangalia, mbali ya udhaifu wa chama, bali pia udhaifu wa mgombea. Na sisi tunafuatilia kwa makini sana.

“Mwisho wa siku, watalazimika kuzunguka kumnadi mgombea wao watakayempitisha, na hapo ndipo tutawauliza nyinyi si ndio mlisema huyu ana udhaifu huu? Kwa kweli ni advantage kwa wapinzani.” Hata hivyo, Zitto alikuwa na mtazamo chanya kuhusu hali inavyoendelea katika harakati za Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba.

“Kwa kweli huu ni mjadala healthy (wenye manufaa) na wapinzani hatuna budi kujifunza kuwa kuna haja ya kupanua demokrasia na kwamba tunapoingia kwenye uchaguzi, lazima tutoke tukiwa wamoja.” Katibu wa Kanda ya Dar es Salaam wa Umoja wa Wamiliki wa Shuke na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Moses Kyando hakuona kama kuna jipya katika mikakati inayotangazwa na makada hao.

“Sidhani kama kuna jambo jipya, wengi hawana jipya,” alisema Kyando.

“Nilichosikia ni matumizi ya lugha za kuwavutia wananchi, ili viongozi hao waingie madarakani, na si vingivevyo.” Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Daniel Kitwana alisema wote waliojitokeza hawawezi kutekeleza mambo wanayosema kwa kuwa watalazimika kufuata mfumo wa chama, ambao umeonyesha kushindwa.

Alisema kwa miaka zaidi ya 50 serikali chini ya CCM imeshindwa kuboresha elimu na kuondoa rushwa, hivyo si rahisi kama ambavyo baadhi ya wagombea wanavyojinadi kwa wananchi.

“Mtu anayeweza kuleta maendeleo katika nchi hii lazima atoke nje ya CCM, Rais Jakaya Kikwete wakati anaingia madarakani mwaka 2005 alibeba matumaini ya Watanzania wengi, lakini kadri siku zinavyokwenda matumaini yanazidi kwisha,” alisema Kitwana.

Aliongeza kuwa hata baadhi ya wagombea waliotangaza kuwa watawaletea maendeleo wananchi kwa kuwa wanachukia rushwa hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa watakapoingia madarakani watamezwa na mfumo wa chama.

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi, Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Modest Mfilinge alisema zaidi ya asilimia 50 ya waliojitokeza wanafaa kuiongoza Tanzania, japokuwa wana kazi ya kurejesha imani ya wananchi iliyobomolewa kwa rushwa.

“Nchi inayumba kutokana na rushwa, kiongozi anayekuja lazima aweke marafiki kando, aunde baraza la mawaziri lenye mchanganyiko wa damu ya vijana na wazee, aache kusema huyu alinifanyia sijui nini,” alisema Mfilinge.

Baadhi ya makada walishatangaza nia mapema, lakini hali ilichangamka baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwaachia huru wanachama sita waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa kosa la kuanza kampeni mapema.

Miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia au wanaotajwa kuwa wataingia kwenye mbio za urais wameshatajwa kwenye kashfa kadhaa zilizoikumba Serikali ya Awamu ya Nne, ambazo ni pamoja na Operesheni Tokomeza Ujangili, ubadhirifu ulioibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), mkataba wa umeme wa dharura na kampuni ya Richmond, uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na EPA.

Hata hivyo, karibu wagombea wote wameahidi kupambana na rushwa, wakisema ndilo tatizo kubwa linalosumbua utekelezaji wa mikakati ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.

Mikakati ya wagombea wengi ni kuinua kilimo, kuboresha elimu, uchumi wa viwanda, kuchochea ubunifu ili kuwezesha vijana kujiajiri na wameahidi kufanikisha hayo kwa kuwa na uongozi imara, kupambana na rushwa, kusimamia maadili na kusimamia mapato. 


Waliojitokeza hadi sasa ni Lowassa, Wasira, Mwigulu, Samuel Sitta, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Mohamed Gharib Bilal, Balozi Ali Karume, Balosi Amina Salum Ali, Luhaga Mpina, Profesa mark Mwandosya, Dk John Magufuli

No comments:

Post a Comment