Alikiba akiwa jijini Los Angeles Marekani na wasanii pamoja na watu mbalimbali walioshiriki kutengeneza video ya wimbo wa kupinga ujangili wa tembo inayotarajiwa kutoka mwezi ujao. Video hiyo imeratibiwa na Wildaid na kudhaminiwa na Swiss Air pamoja na Pembe Club.
Katika kutimiza jukumu lake jipya kama balozi wa kimataifa wa Wildaid, shirika la kimataifa la uhifadhi wanyamapori, mwanamuziki maarufu Mtanzania – Alikiba amesafiri kuelekea jiji la Los Angeles nchini Marekani ili kutengeneza video ya kupinga ujangili kwa tembo wa Tanzania akishirikiana na baadhi ya watengeneza filamu maarufu wa Hollywood.
Video hiyo ambayo imesimamiwa na mtengeneza filamu maarufu Kevin Donovan itatoka mwezi ujao ikiwa ni sehemu ya kampeni iliyozinduliwa jijini Dar es salaam mwaka huu kupinga ujangili wa kuua tembo ikijulikana kama “Ujangili Unatuumiza Sote”.
Kampeni hiyo ilizinduliwa kwa ushirikiano wa Wildaid na African Wildlife Foundation, mashirika ya kimataifa ya uhifadhi wanyamapori na maliasili ambayo yanafanya kazi pamoja kwenye mabara ya Afrika na Asia kupunguza ununuzi wa bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu na kuhamasisha umma juu ya janga la ujangili. Wimbo wa Alikiba umelenga kuwalinda na kuwafurahia Tembo, mnyama aliyeko kwenye hatari ya kutoweka.
Wimbo huo mpya wenye lengo la kuhamasisha vijana katika kuwalinda na kuwapenda tembo umetengenezwa na kurekodiwa na Brian Rumsey na kusimamiwa na Oththan Burnside ambaye ameishafanya kazi na wasanii kama Rihanna na Sean Paul. “Sisi kama Watanzania tunatakiwa kujivunia wanyama hawa wazuri ambao wanauwawa na majangili kila siku,” alisema Alikiba. Kampeni hii imelenga kuhamasisha Watanzania kujivunia wanyamapori wetu na kupambana na wote wanaoua tembo kila siku kwa ajili ya pembe zao.”
Mradi huu umeratibiwa na Wildaid na kudhaminiwa na shirika la ndege la SwissAir huku kampuni ya Pembe Club ya Los Angeles inayotengeneza vito vya madini mbalimbali na kutumia faida yake kusaidia harakati za uhifadhi wanyama pori ikidhamini onyesho la Alikiba lililofanyika mwisho wa wiki kwenye jiji hilo ambapo jumla ya dola milioni 2.5 zilichangwa na wahisani kusaidia jitihada za kupinga ujangili wa tembo.
No comments:
Post a Comment