Mchuano wa kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la 11 imebaki kwa vigogo wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vikao vya chama vya kupitisha jina moja vikisubiri Mwenyekiti, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.Chanzo cha uhakika ndani ya CCM kimeieleza kuwa, walioonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ni aliyekuwa Spika wa Bunge la 10 Ni Anne
Makinda, aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la 10, Mussa Azzan Zungu na Mjumbe wa Kamati kuu Dk. Emmanuel Nchimbi.Mmoja wa wanaotajwa kugombea nafasi hiyo, Job Ndugai ameithibitishia Nipashe kuwa atawania nafasi hiyo na anaomba wabunge wote kumuunga mkono kwa kuwa uzoefu, uwezo na elimu yake vinamuwezesha kushika nafasi hiyo nyeti.
Alisema anasubiri chama chake (CCM) kikamilishe taratibu zake na kuruhusu wagombea wa nafasi hiyo kuchukua fomu ndipo atafanya hivyo kwa kuwa ana sifa zote za kuwania nafasi hiyo.
Ndugai ambaye ni Mbunge Mteule wa Jimbo la Kongwe, alisema wabunge wa Bunge la 11 wana uwezo, hivyo ni wazi hawatahitaji Spika kutoka nje yao na mwenye uwezo wa kuongoza Bunge hilo ni yeye.
Alisema iwapo Spika wa Bunge la 10, Makinda atasimama kuwania tena nafasi hiyo hana tatizo naye na kumuomba kumuunga mkono iwapo jina lake (Ndugai) litapenya ndani ya chama na kufika bungeni.
“Naamini kuanzia kesho (leo) chama changu kitatoa utaratibu wa uchunguaji fomu, ni kweli nina nia ya dhati kabisa ya kugombea nafasi hiyo ya juu katika muhimili wa Bunge na ninaomba niungwe mkono,” alisema.
Naye, Dk. Nchimbi, alipopigiwa simu na Nipashe, alimweleza mwandishi kuwa CCM bado haijatangaza nafasi zilizo wazi zinazostahili kugombewa.
Hata hivyo, alipoulizwa kama atagombea nafasi hiyo hakukubali wala kukataa na kumtaka mwandishi kusubiri utaratibu utakaowekwa na chama.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhwavi, alipoulizwa kuhusiana na mchakato wa kumtafuta mgombea wa uspika, alimtaka mwandishi kuzungumza na Katibu wa Sekretarieti ya CCM, Anamringi Macha, ambaye alisema vikao vya CCM kujadili na kumpanga suala hilo bado havijafanyika.
“Vikao vinamsubiri mwenyekiti ndiyo wataamua fomu zianze kutoka lini na mchakato mzima kwa ujumla,” alisema Macha.
Ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chadema, NLD, NCCR Mageuzi na Cuf, bado haijajulikana vikao vya kujadili suala hilo vitafanyika lini.
Wenyeviti wenza wa umoja huo, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema wala James Mbatia, Mwenyekiti NCCR-Mageuzi hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bunge la 10, Tundu Lissu, aliieleza Nipashe kuwa hakuna kikao chochote cha Ukawa kilichokaa kujadili suala hilo hivyo ni vigumu kuzungumzia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment