Yanga imeanza rasmi mazoezi yake leo asubuhi kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume uliopo kwenye ofisi za TFF Ilala jijini Dar es Salaam tayari kujiandaa na michuano mbalimbali inayoikabili ikiwemo ile ya Kagame Cup, ligi kuu Tanzania bara pamoja na michuano ya klabu bingwa barani Afrika.
Mazoezi hayo yameongozwa na kocha mkuu wa Yanga Hans van der Pluijm akisaidiwa na kocha wa makipa Juma Pondamali na viongozi wengine wa benchi la ufundi la timu hiyo ambayo ndio mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa msimu uliomalizika hivi karibuni.
Wachezaji saba tu ndiyo walikuwepo kwenye mazoezi ya leo huku wachezaji wengine wakiwa kwenye timu zao za taifa wakati wengine wanatarajiwa kuanza kuingia nchini kuanzia leo kujiunga na wachezaji ambao tayari wamesharipoti kwenye timu.
Deus Kaseke ni miongoni mwa wachezaji waliofanya mazoezi leo asubuhi huku van Pluijm akionekana kumpa maelekezo binafsi mara kwa mara wakati wote wa mazoezi. Walikuwepo pia wachezaji wawili wa kigeni ambao uongozi haukutaka wafanyiwe mahojiano na vyombo vya habari wakidai wakati wa kufanya hivyo bado haujafika.
Wapenzi na mashaki wa Yanga wamejitokeza kwa wingi kuishuhudia timu yao ikifanya mazoezi ikiwa ni mara ya kwanza tangu kumalizika kwa ligi kuu Mei 9 mwaka huu. Mazoezi yataendelea tena kesho huku wachezaji wengine wakitarajiwa kuongezeka tofauti na ilivyokuwa leo.
No comments:
Post a Comment