Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekanusha taarifa zilizo zagaa mitaani kwamba, limekubali kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara kutoka wachezaji watano hadi hadi kufikia wachezaji saba.
Katibu mkuu wa TFF Selestnine Mwesigwa amesema, hakuna ukweli wowote juu ya taarifa hizo kwasababu mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na TFF kuhusu madai ya ongezeko la wachezaji wa kigeni kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
“Huo siyo ufanyaji kazi wa TFF, TFF tunapofanya maamuzi huwa tunatoa taarifa kwa ‘press release’ au kamati ya utendaji inatoa tamko kwahiyo sijui chanzo cha habari hizo. Kamati ya utendaji haijapitisha jambo kama hilo na sidhani kama kuna kiongozi wa TFF ambaye ametoa tamko hilo.”, amesema Mwesigwa.
“Vyombo vya habari sio vyombo vya TFF kama angekua ni afisa habari wa TFF au kurugenzi yenyewe ya habari ningesema sawa, lakini si TFF na kama sio sisi basi wenyewe wanajua wametoa wapi habari. Hakuna siri, ingekuwa imepita ingetangazwa lakini kwa vile jambo halijatangazwa basi halijapitishwa, kanuni za mashindano bado hazijatoka zikitoka tutajua na kanuni zinajumuisha mambo mengi sana zina ‘guide’ mambo mengi sana kuanzia ligi kuu, daraja la kwana na kadhalika”, Mwesigwa alifafanua.
Kwa maana hiyo, sasa idadi ya wachezaji wa kigeni bado inaendelea kusalia ileile ya wachezaji watano licha ya kuwepo na taarifa za kuwepo na ongezeko la wachezaji wengine wawili wa kigeni na kufikia wachezaji saba.
Mwishoni mwa juma lililopita kulikuwa na taarifa zinazodai kuwa, huenda idadi ya wachezaji wa kigeni ikaongezeka kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa msimu ujao wa 2015-2016 lakini tayari TFF imetolea ufafanuzi jambo hilo kupitia kwa katibu mkuu wake Selestine Mwesigwa.
No comments:
Post a Comment