Kamati ya usajili ya ‘Wekundu wa Msimbazi’ kupitia kwa mwenyekiti wake wa usajili Zacharia Hans Poppe, imetangaza kumpata kocha mpya kwa ajili ya kukinoa kikosi cha Simba SC akirithi mikoba ya kocha Goran Kopunovic ambaye aligoma kusaini mkataba mpya akidai dau nono ambalo Simba walishindwa kumpatia
Poppe amesema wamepata kocha mpya raia wa Uingereza kwa ajili ya kuendelea pale alipoishia Kopunovic na watamtangaza rasmi pindi atakapokuwa amesaini mkataba kwa ajili ya kukinoa kikosi cha wanamsimbazi.
“Kuhusu suala la kocha tayari tumelimaza, tunasubiri asaini mkataba kwanza, tumeshakubaliana kila kitu na tumemtumia mkataba. Sio Kim Paulsen kama wengi wanavyodhani, japo tulifanya mazungumzo na Kim lakini tayari alikuwa na timu ambayo anaifundisha akashindwa kuiacha kuja kujiunga na sisi”, amesema Poppe.
“Kocha anatoka Uingereza na atakapokuwa amesaini tu ule mkataba tuliomtumia tutaweka wazi kila kitu, lakini wanasimba washike tu suala la kocha tayari limeshamalizika”, ametamba Poppe.
Kopunovic alitua Simba kuchukua nafasi iliyoachwa na Ptrick Priri aliyetimuliwa kunako kikosi hicho baada ya mfululizo wa matokeo mabaya kwenye mechi za mwanzo za ligi kuu. Kopunovic ambaye ni raia wa Serbia alisaini mkata wa miezi sita ambapo mkataba wake ulimalizika mara tu baada ya kumalizika kwa ligi kuu Mei 9 mwaka huu na Yanga kutwaa taji hilo. Simba ilishindwa kufikia makubaliano na kocha huyo hivyo wakamwachia aende zake na kuanza kuasaka kocha mwingine wakuchukua nafasi hiyo.
Akizungumzia suala la ushiriki wa Simba kwenye michuano ya Kagame Cup Poppe amesema, hadhani kama timu yao itashiriki mashindano hayo kwasababu mpaka sasa timu bado haijakusanywa kwa ajili ya kuanza mazoezi na hawawezi kupeleka timu ambayo hajajitayarisha, lakini akaongeza kuwa, mpaka sasahivi bado hawajapokea mwaliko rasmi kutoka kwa waandaaji wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment