Baada ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya serikali ya Kampala na Pyongyang kudumu kwa muda mrefu, hatimaye Uganda imewataka askari wa nchi hiyo kuondoka haraka katika ardhi yake.
Korea Kaskazini na Uganda zilitiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi mnamo mwaka 1987, uhusiano ambao ulikuwa ukiongezeka muda kila mara.
Hata hivyo Kampala imetangaza kuwa haina haja ya kuendelezwa makubaliano ya ushirikiano huo na Pyongyang.
Kwa mujibu wa duru za ndani nchini Uganda, karibu washauri 50 hadi 60 wa Korea Kaskazini wako nchini humo, na kwa hivyo maafisa hao wa kijeshi watatakiwa kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo haraka kufuatia amri ya serikali.
Uamuzi wa kuwatimua maafisa wa jeshi wa Korea Kaskazini, umekuja kufuatia safari ya hivi karibuni ya Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini nchini Uganda, ambapo aliwataka viongozi wa Kampala kutekeleza vikwazo vya kimataifa dhidi ya jirani yake Korea Kaskazini.
Akiwa nchini Uganda, maafisa wa nchi hiyo walimthibitishia rais huyo azma yao ya kukata uhusiano wa kijeshi na Korea Kaskazini haraka iwezekanavyo.
USISAHAU KULIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment