What's Trending?

Labels

Ads

Sunday, July 26, 2015

Yanga kuikwepa , kuifuata Azam

   Wachezaji wa timu ya Yanga
Yanga inaingia uwanjani kuikabili timu ngumu ya Al- Khartoom ya Sudan leo katika mchezo wa kukamilisha ratiba, lakini wenye kutoa msimamo halisi wa Kundi A la Mashindano ya Kagame.
Mchezo mwingine utakuwa baina ya Gor Mahia dhidi ya Telecom utakaoanza saa 8.00 mchana kwenye Uwanja wa Taifa,
Viajana hao wa Jangwani wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita, wanatanguliwa na Al-Khartoum inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba, sawa na Gor Mahia ya Kenya, huku KMKM ya Zanzibar yenye pointi tatu tayari imeaga mashindano hayo pamoja na Telecom ya Djibouti inayoshika mkia bila kuwa na pointi.
Yanga, yenye safu kali ya ushambuliaji imegeuka kinara wa kukosa mabao kwenye mashindano hayo na endapo itashinda leo na Gor Mahia kufungwa kimaajabu au kutoa sare na Telecom, itaongoza kundi lake na itakutana na Al- Malakia ya Sudani Kusini iliyopita kama ‘mshindwa bora’.
Endapo Yanga itafungwa na Al Khartoum itabaki katika nafasi ya tatu na itaikabili APR ya Rwanda kwenye robo fainali na kama itashinda leo, halafu Gor Mahia ikashinda, basi Yanga itakamata nafasi ya pili kwenye kundi lake na itacheza na Azam kwenye robo fainali itakayopigwa Jumatatu na Jumanne.
Kwa sababu hizo, Yanga itabidi ifanye kazi ya ziada kuifunga Al- Khartoum iliyoonyesha soka safi kwenye mashindano mwaka huu na kuonekana moja ya timu ngumu baada ya kuwabana Gor Mahia juzi na kutoka sare bao 1-1.
Kocha mkuu wa Yanga, Hans Pluijm itabidi akae na safu yake ya ushambuliaji na kuituliza, iache papara kwani ilikosa mabao mengi katika mchezo uliopita dhidi ya KMKM. Pia, mawinga wa timu hiyo wanatakiwa kuwasaidia viungo wa kati, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima, hasa timu yao inapokuwa haina mpira kwani mara nyingi wamekuwa wakicheza pembeni na kuifanya timu hiyo kuzidiwa eneo la katikati ikikutana na timu iliyojaza viungo wengi katikati.
Pia, Yanga imekuwa na tatizo la wachezaji wake kukaba pindi timu hiyo inapokuwa haina mpira kwani kazi kubwa wamekuwa wakifanya mabeki wa timu hiyo, huku wachezaji wengine wakionekana kutegea, jambo ambalo limekuwa likiwagharimu mara kwa mara na mchezo.
Wachezaji pekee wa mbele wanaojitahidi kukaba ni Deus Kaseke na Amissi Tambwe. Kila wakati, Pluijm ameonekana akizozana na wachezaji wake, hasa washambuliaji kutokana na kuchukizwa na jinsi wanavyokosa mabao ya wazi, lakini pia amekuwa mkali kwa mawinga ambao wamekuwa hawarudi katikati kuwasaidia viungo pindi timu inapokuwa ina mpira au haina mpira.
Hata hivyo, Pluijm amefurahishwa na kikosi chake kutinga robo fainali huku akitaka kuhakikisha wanashinda mchezo wa leo na kuongoza kundi lao na hana hofu na timu yoyote atakayokutana nayo kwenye robo fainali. “Kadiri siku zinavyoenda kikosi changu kimekuwa kikiimarika, tunacheza na Al-Khartoum Jumapili (leo), nimewaona katika mechi kadhaa ni wazuri na wagumu, hivyo hatuna budi kujipanga kuhakikisha tunashinda.
Kocha wa Al- Khartoum, James Kwesi Appiah alisema anajua anakutana na Yanga ambayo ni timu nzuri na ngumu na iko uwanja wa nyumbani, lakini malengo yao ni ushindi na kuhakikisha wanafika fainali katika mashindano haya na kutwaa ubingwa uliokuwa ukishikiliwa na ndugu zao, El- Merreikh ambao hawakushiriki kwa sababu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

No comments:

Post a Comment