Asha - Rose Shaban Mtengeti Migiro ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliochukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na chama hicho tawala kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Migiro ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi, amewahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na sasa ni Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba.
Ndugu wanamzungumziaje?
Kaka wa Dk Migiro, Ally Shaban anasema dada yake huyo ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya mzee Shaban Mtengeti, yenye watoto kumi. Mtengeti alikuwa chifu wa Usangi, enzi za mkoloni hadi kwenye miaka ya 1960, Mwalimu Nyerere alipofuta uchifu.
Anasema tangu alipozaliwa, Dk Migiro amekuwa ni mtu wa watu asiyekuwa na makuu. “Anapenda watu na mtu asiyependa kuonewa,” anasema.
Kaka huyo anaendelea kueleza kuwa Dk Migiro ana nyota ya uongozi kwa kuwa ameanza kuongoza tangu alipokuwa chuo kikuu, ambako alikuwa mbunge kwenye Baraza la Vyuo.
Nafasi ya mwanamke katika uongozi
Ally anaeleza kuwa Dk Migiro ni mwanamke jasiri anayependa kusimamia haki na aliweza kuongoza Umoja wa Mataifa, hivyo anaweza pia kuongoza Tanzania.
Ally anasema uongozi wa mwanamke unasimamia sheria zaidi tofauti na uongozi wa mwanamume ambao wengi wameonekana wakipindisha sheria na kufichiana maovu kwa kigezo cha kulindana.
Wakazi wa Usangi wamzungumzia
Huwezi kuamini kwamba wakazi wengi wa Usangi hawamfahamu Dk Migiro kwa sura, huo ndio ukweli na baadhi wamesema hilo limetokana na daktari huyo wa falsafa za sheria kuishi muda mwingi jijini Dar es Salaam.
Migiro ameishi zaidi nje ya Mwanga kwa sababu mama yake ni mtu wa Dar es Salaam na kwa kiasi kikubwa amelelewa na mama na Mwanga alifika baada ya kifo cha baba yake.
chanzo ni gazeti la Mwananchi june 18,2015
chanzo ni gazeti la Mwananchi june 18,2015
No comments:
Post a Comment