What's Trending?

Labels

Ads

Thursday, June 11, 2015

KENYA: MWANAMUME AMUOMBA UHURU RUHUSA APANDE MIRAA IKULU

MTAFUNAJI mmoja wa miraa mjini Meru anataka kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili kuomba ruhusa ya kupanda mmea huo katika Ikulu ya Nairobi.

Rajesh Hirani
Bw Rajesh Hirani akiwa na miraa mjini Meru Juni 10, 2015. Picha/KENNEDY KIMANTHI Bw Rajesh Hirani, ambaye amekuwa mtafunaji miraa kwa miaka mingi, anasema kufikia mwisho wa wiki hii atakuwa ameanza utaratibu wa kufika Ikulu kukutana na Rais Kenyatta kuwasilisha ombi lake.

“Kufikia mwisho wa wiki hii nitakuwa nimeanza mipango ya kufika Ikulu kwa shughuli zangu za kupanda miraa katika makao ya rais,” akasema Bw Rajesh.

Alisema hatua yake hiyo si ya kujitafutia makuu bali inalenga kufufua biashara ya miraa akisema wakulima wa Kaunti ya Meru wameathirika vibaya kiuchumi tangu serikali ya Uingereza ilipopiga marufuku zao hilo nchini humo.

Bw Rajesh, ambaye pia anajiita Green Gold Ambassador (Balozi wa Dhahabu ya Kijani Kibichi) anasema marufuku hiyo imeua biashara ya miraa.

Anasema Rais Kenyatta akimhurusu kupanda mmea huo Ikulu ataondoa dhana ya Wakenya wengi kuwa miraa ni dawa ya kulevya.

Rajesh, mwenye umri wa 37, na mzaliwa wa Meru, anasema masuala yote kuhusu mmea huo yanafaa kuchukuliwa kwa uzito.


Anapanga pia kumuomba Gavana wa Kaunti ya Meru Peter Munya amruhusu kupanda miraa katika makao yake rasmi.

Kampeni yake pia inalenga kusukuma serikali ya Kenya kukabili mashirika ya kimataifa ya nchi zinazochukulia miraa kuwa dawa ya kulevya.

“Tazama nchini Tanzania, miraa ni marufuku pia. Kwa moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Kenyatta anafaa kuzungumza na mwenzake wa Tanzania ili marufuku hiyo iondolewe,” akasema na kuwaomba washikadau wote wamuunge mkono kufanikisha kampeni yake.

Bw Rajeshi, ambaye ametafuna miraa tangu 1994, alikuwa akionekana katika kituo cha biashara cha Makutano (ambacho ni kitovu cha uchumi mjini Meru), akinunua miraa na kugawia marafiki.

Wakati wa mashindano ya magari ya Meru Safari Rally yaliyomalizika majuzi, alivutia wengi kwa kutembea huku amejaza miraa kwenye mifuko yake na kuwahimiza wakazi waombe serikali ipiganie kuondolewa kwa marufuku hiyo.

Ishara muhimu
“Rais akikubali itakuwa ishara muhimu kwa wakulima, akikataa, sitavunjika moyo, nitaendelea kujaribu kwa sababu kwa kweli watu wanateseka,” akasema.

Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya wakazi wa Meru na asilimia 75 ya wenzao wa Nyambene wanatengemea mmea huo kwa mahitaji yao ya kila siku.

Marufuku hiyo pia ilifanya maelfu ya watu, wakiwemo wapakiaji, madereva na wahusika wengine katika biashara ya miraa kupoteza kazi.

Alipotembelea Kaunti ya Meru mnamo Februari mwaka huu, Rais Kenyatta aliwahakikisha wakulima wa miraa kuwa serikali yake imejitolea kuzungumza na Uingereza ili kuondoa marufuku hiyo.

No comments:

Post a Comment