What's Trending?

Labels

Ads

Friday, July 29, 2016

Rais Magufuli Atoa ONYO Kali....."Mimi sijaribiwi, wasije kunijaribu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Julai, 2016 ameanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambapo amezungumza na wananchi kwa lengo la kuwashukuru
kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali katika kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo.


Akiwa Mkoani Singida, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli amewasihi watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye atathubutu kuchochea vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.


“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa.


“Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa” Amesema Rais Magufuli.


Kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano tangu aingie madarakani Rais Magufuli ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya laki moja na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.


Hatua nyingine ni kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini, kutenga shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard gauge na pia akazungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi atakayeendelea kutamba.


Akiwa njiani Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Ikungi na baadaye amefanya mkutano wa hadhara Singida Mjini ambako amesisitiza kuwa serikali yake haiko tayari kumvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa Ahadi na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Singida


29 Julai, 2016

No comments:

Post a Comment