What's Trending?

Labels

Ads

Thursday, November 12, 2015

KIMENUKA..Maduka ya Dawa Karibu na Hospitali zote za Serekali Kuondolewa

SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha maduka ya dawa katika hospitali zake zisizokuwa nayo na kuweka maduka mapya ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), hatua itakayohakikisha dawa zinapatikana katika hospitali hizo.
Aidha, imesema ili kufanikisha hilo, inafanya mazungumzo na wamiliki binafsi wa maduka ya dawa yaliyo nje ya hospitali zote za serikali ili yahamishwe kuondoa mgongano wa kimaslahi baada ya kubaini maduka mengi ni ya watumishi wa afya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando, aliyasema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kufafanua zaidi kwa simu alipozungumza na gazeti hili baada ya ziara hiyo.

Dk Mmbando alisema changamoto ya dawa ipo katika maeneo mengi ya nchi, hivyo serikali imeandaa utaratibu wa kuweka maduka ya dawa ya serikali ndani ya hospitali zake ambayo yatasaidia upatikanaji wa dawa kwa wepesi na kwa bei rahisi. “Maduka ya dawa hayapo katika hospitali zote.

Tuliruhusu kuwepo kwa maduka binafsi ili kuongeza ushindani wa dawa, lakini baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanawaandikia wagonjwa dawa wanazojua katika duka la hospitali hakuna, na kumwagiza aende duka la nje ambalo ni lake ama la mwenzake.

“Mpango tunaouzungumza hapa ni kuweka maduka katika hospitali za serikali zisizo nayo na pia kuanzisha maduka ya MSD ndani ya hospitali moja kwa moja ili kuhakikisha dawa stahiki zote zinapatikana kwa wakati,” alifafanua Dk Mmbando.

Alisema hatua hiyo itaondoa ucheleweshwaji wa kupata dawa kwa wakati na itaongeza ufanisi. Kadhalika alisema hivi sasa utekelezaji wa mpango huo unaendelea hatua kwa hatua. “Hilo suala limezungumzwa vizuri pia katika bajeti tunayoitekeleza katika mwaka huu wa fedha (2015/2016) na tutaeleza utekelezaji wake mwakani,” alisema Dk Mmbando.

“Wananchi wamekuwa wakilalamika kukosa dawa ndani ya hospitali na kutakiwa kununua katika maduka ya nje, jambo ambalo limeleta sintofahamu kwa wananchi, hivyo kwa sababu maduka yote ya dawa yamesajiliwa kisheria tunataka kuyaondoa kwa maana ya kuyahamisha ili kuondoa huo mgongano,” alibainisha Dk Mmbando.

Katika hatua nyingine, Serikali imezitaka hospitali zake zote nchini kuhakikisha zinatenga bajeti itakayowasaidia kufanya marekebisho ya vifaa tiba pindi vitakapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.

Dk Mmbando alisema hospitali hizo zinapaswa kuweka bajeti ya vifaa tiba itakayowasaidia wao kama hospitali kufanya marekebisho na kuacha kusubiri mpaka serikali itoe fedha za marekebisho ya vifaa hivyo.

“Hospitali hizi tunajua zinapata fedha, hatutegemei kusikia malalamiko ya vifaa kuharibika, lazima wachukue hatua wao wenyewe za kuhakikisha vifaa vinarekebishwa ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa na kuwanyima haki ya msingi ya kupatiwa huduma bora,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Alisema amefurahishwa na utoaji huduma katika Hospitali ya Ocean Road licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa dawa za saratani. “Hospitali inafanya huduma kwa ushirikiano, wafanyakazi wanafanya kazi kama timu, jambo ambalo limenipa nguvu,” alisema na kuaigiza MSD kuhakikisha wanahifadhi dawa za kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa saratani ili kusaidia wagonjwa hao kupata huduma bila kuwepo vikwazo.

Pia aliwataka wakurugenzi wa Idara ya Tiba na Famasia waliopo wizarani watunze asilimia ya fedha kwa ajili ya kununua dawa za wagonjwa wa saratani. Dk Mmbando alisema serikali pia imeandaa mwongozo wa huduma za tiba ambao utatumika katika hospitali za umma utakaosaidia kujua gharama za matibabu kwa wananchi.

“Mwongozo huo umekamilika katika rasimu ya kwanza tunasubiri waziri atakayekuja aweze kupitia, kuuzindua na kutangazwa rasmi,” alisema Dk Mmbando. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Ocean Road, Diwani Msemo alisema amefurahishwa na ujio wa Katibu Mkuu huyo, kwani amekuwa na maagizo mazuri ambayo yanalenga kusaidia hospitali hiyo.

Pia alisema maagizo ya Katibu kuhusu upatikanaji wa dawa yatawasaidia kwani wamekuwa na changamoto kubwa ya dawa, jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa wagonjwa.
USISAHAU KULIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPA CHINI                                                                                        

No comments:

Post a Comment