Charles Raphael anayedaiwa kumnyonga mke wa mtu gesti.
MAPYA tena! Yale mauaji ya mke wa mtu, Ashura Maulid yaliyotokea kwa kunyongwa gesti na mwanaume anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake wa kwenye mtandao wa kijamii Facebook, Charles Raphael (pichani), sasa picha yake imepatikana na mengine yameibuka.
MTUHUMIWA WA MAUAJI
Taarifa kutoka chanzo makini zimeeleza kuwa, mwanaume huyo mpaka anafikwa na tukio hilo la kudaiwa kumuua mwanamke huyo kwa kumnyonga alikuwa akijihusisha na kazi ya ubaharia kwa safari za ndani na nje ya nchi hasa Yemen ambapo alikuja nchini kuchukua vyeti vyake ili akaajiriwe rasmi nchini huko.
VYANZO VYA POLISI
Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi katika maelezo ya mtuhumiwa huyo, inadaiwa siku ya tukio, wawili hao walikubaliana wakutane kwenye gesti hiyo na kufanya mapenzi.
“Walifanya mapenzi kweli tena bila kinga. Walipomaliza, mwanaume alipekua mkoba wa mwanamke, akakuta vidonge ambavyo yeye alivitafsiri kwamba ni vya kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi (ARV).
MZOZO WAIBUKA
“Mzozo ulianza kuibuka. Mwanaume alimjia juu mwanamke kwamba huenda amemwambukiza virusi vya Ukimwi ingawa mwanamke alijitetea kuwa vidonge vile siyo ARV. “Kwa hasira mwanaume akamshika shingoni na kumkaba, kisha akamwachia na yeye akaondoka,” kilisema chanzo.
Kikaongeza: “Wakati mwanaume anaondoka kwa hasira, mwanamke alikuwa ameanguka chini lakini alikuwa hajafariki dunia. “Ndipo nyuma, wahudumu wa gesti walibaini kuwa, ndani ya chumba hicho kuna mwili wa mwanamke ukiwa chini na kutoa taarifa polisi.”
MTUHUMIWA ALIKAMATWAJE?
Habari zaidi zinadai kuwa, baadhi ya wafanyakazi wenzake marehemu walijua wawili hao walikuwa pamoja kwa hiyo kifo cha mwenzao walikihusisha na mwanaume huyo.
“Ili kumpata mtuhumiwa, polisi walimtumia mfanyakazi mmoja wa marehemu ambaye aliwahi kutongozwa na mwanaume huyo siku za nyuma. Yeye alimpigia simu mwanaume na kumwambia yuko tayari kwa sasa kumpa penzi. Jamaa akafurahi, wakapanga kukutana maeneo ya Jeti, Dar es salaam ambapo mtuhumiwa huyo alipofika, polisi walimkamata.
Habari zinasema kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa huku akiwa hajui chochote, akiwa ndani ya gari la kukodi aina ya Toyota Carina (namba zinahifadhiwa) na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar (anakoshikiliwa hadi sasa).
Marehemu Ashura Maulid enzi za uhai wake.
NDANI YA KITUO CHA POLISI
“Alipofikishwa kituoni aliambiwa kuwa ameua mwanamke kwa kumnyonga, akashtuka sana. Akasimuliwa mkasa wote na yeye akajieleza,” kiliongeza chanzo.
POLISI WAVIFANYIA KAZI VIDONGE
Habari zaidi zinawekwa wazi kwamba, polisi walivichukua vidonge hivyo na kuvipeleka kwa wafamasia kwa ukaguzi kama kweli ni ARV lakini vikabainika ni vya minyoo.
MUME WA MAREHEMU
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, siku ya tukio mume wa marehemu, Suleiman Othman alimpigia mkewe simu ili kujua alipo akamwambia anatoka kazini lakini kutokana na foleni za barabarani atachelewa kufika nyumbani.
Taarifa zaidi zinadai kwamba mume alipoona usiku unazidi kuingia, mkewe hajarudi alimpigia simu ambapo iliita bila kupokelewa baadaye ikawa haipatikani hewani.
TAHADHARI KWA WATUMIA FACEBOOK
Polisi mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa vile siyo msemaji, alisema kumekuwa na kesi nyingi kwenye vituo vya polisi ambapo chanzo chake ni Facebook.
“Mimi nawaambia watumiaji wa Facebook kujihadhari na mawasiliano na watu wasiowafahamu, hasa kwenye suala la uhusiano wa mapenzi,” alisema afande huyo.
TUJIKUMBUSHE
Tukio hilo lilijiri Mei 19, mwaka huu kwenye nyumba ya kulala wageni (guest house) iliyopo maeneo ya Afrikasana, Dar pembezoni mwa barabara ya kwenda Kijitonyama kupitia Polisi Mabatini.
Katika habari hiyo, mume wa marehemu alisema haamini kama mkewe alishawishika kukutana na mwanaume huyo kwa ajili ya kufanya mapenzi tu bali alikuwa na nia ya kumwibia pesa za mauzo ya siku hiyo.
Alisema mkewe alikuwa akifanya kazi ya kuuza mafriji kwenye duka moja lililopo maeneo ya Afrikasana, Dar.
No comments:
Post a Comment